Thursday, August 28, 2014

David Aidani Mjanja,makala,,, tukio la kufukiwa mbuzi katikati ya uwanja wa jangwani wakati wa mechi ya watani wa jadi,nilikuwepo.




David Aidani Mjanja ni miongoni mwa  washambuliaji maili  ambao waliwahi tokea na waliwika sana hapa nchini mnamo miaka ya 1990 -2005,katika club tofauti za ligi kuu hapa nchini,na Timu ya Taifa.

Mjanja ambaye ni mtoto wa saba katika familia yenye watoto 8 alizaliwa mwaka 1973 katika Kijiji cha Mdemu mkoani Dodoma, katika maojiano maalum ameeleza mengi na kufafanua historia ya maisha yake ya soka kwa kina;


 David mjanja wapili toka kushoto [waliosimama]

“nilianza kucheza mpira katika shule ya msingi mndemu huko Dodoma ,na baada ya kuhitimu elimu ya shule ya msingi nikajiunga na chuo cha ufundi Makenika N V T C,kwa sasa ni chuo cha Veta,baada ya kuitimu nilipata ajira katika kiwanda cha Mazuria Morogoro,hapo ndipo nyota yangu ilipoanza kunga’aa na nikafanikiwa kupata nafasi ya kuitumikia timu ya mkoa wa Morogoro.

“Ushirika ya Moshi walivutiwa na uwezo wangu wa kusakata kabumbu nikiwa na timu ya mkoa wa Morogoro ambapo 1991 nikajiunga na timu hiyo hapo nilidumu hadi 1994  ndipo nilipoamua kutimukia Yanga timu ambayo ilikuwa ikisaka saini yangu kwa udi na uvumba kwa kipindi kirefu wakati nikiwa na timu ya Ushirika.

Sababu za kuongoka Yanga

“Nilipenda toka moyoni kuchezea Yanga kwa kipindi Kirefu lakini ilinilazimu kuondoka kwa shingo upandi mara baada ya kukwaruzana na moja wa kiongozi ambaye alikuwepo katika kamati ya usajiri kwa sababu ambazo mimi mwenyewe adi leo hii sizifahamu.


“nakumbuka niliambiwa kuwa tayari jina langu limeshawekwa kwa ajili ya kusainishwa mkataba mwingine,lakini yule kiongozi akaamua kulikata jina langu na kumweka mchezaji ambaye alikuwa amemtafuta yeye mwenyewe ili kuniondoa kwa maslai binafsi iliniuma sana na mwaka 1997 nikaamua kutimukia  Maji Maji ya Songea.


“Wakati nikiwa Maji Maji maisha yalikuwa mazuri kwa kuwa Maji Maji ya kipindi kile ilikuwa na uongozi imara nikacheza pale hadi 2000 Prisons wakaniona kutokana na uwezo wangu wa kupachika mabao na wakaamu kunichukua, ambapo nilichezea Prisons hadi 2005 hapo ndipo nikafikiria kustaafu soka.

“Lakini kwa kipindi hicho Prisons walikuwa na Tawi la Timu yao Tanga ambalo iklifahamika kwa kwa jina la Small Prisons wakaamua kunipereka Tanga ambako niliendelea kutumikia Timu hiyo.


“Baada ya kuitumikia timu Hiyo kwa misimu mitatu hapo ndipo nikaona uwezo wangu wa kusakata kabumbu umefikia kikomo na mwaka 2008,nikatangaza kutundika Daruga,na kuyapa kisogo mambo yote yahusuyo kandanda.


Hawezi kusahau

“Mwaka 1995,katika meshi ya watani wa jani Simba na Yanga wakati mimi nipo Yanga kuna tukio lilifanyika Usiku wa manane katika uwanja wa jangwani unaweza usihamini lakini siku hiyo alichukuliwa mbuzi mzima na kufukiwa katikati ya uwanja ili kuwaloga Simba.

“Tukio hilo ambalo lilifanyika ndani ya Dakika kumi na Tano,alichukuliwa mbuzi Mzima huku akiwa amezibwa kwa Pamba katika maeneo yote ambayo yanatoa Hewa huku kila mchezaji akiwa na mganga wake binafsi pakachimbwa shimo huku zikinyunyizwa dawa na kumfukia yule Mbuzi.


“wakati tukiendelea kupewa dawa zingine wale waganga walitupa masharti na kutuambia kuwa mtu yeyote atakayetoa siri na kupokea pesa kwa ajili ya kuhujumu timu atakutwa na Adhabu kali Sana.

“Asubuhi tukaamka na tukajiandaa na mchezo,wakati wa mechi ulipofika tukaingia uwanjani kwa kweli mchezo ulikuwa mgumu sana kutokana na umahili wa Simba ya kipindi kile Hadi mwamzi wa katikati alipopuliza kipenga kuhahiria dakika 90 za mchezo zimemalizika Simba 1,Yanga 0 bao ambalo lilipachikwa kimiani na Dua Saidi,siwezi kusahau.

“Nakumbuka wachezaji wa Yanga walikuwa Steven Nemes,Kenny Mkapa,Salumu Kabunda,Wille Martin,Method Mogela,Said Mwamba,Mohamed Husein,Edbili Lunyamila,David Mjanja Pamoja na Sanifu Lazaro,ambayo licha ya maandalizi ambayo timu yetu iliyafanya ndani na nje ya uwanja tulitoka uwanjani tukiwa vichwa chini.

“Kiukweli ushirikina hauna mchango wowote katika mpira zaidi ya mazoezi na na kujituma uwanjani, lazima nchi zetu za kiafrika zibadilike kama tunataka kufika mbali kisoka na pawepo na viongozi na sio watawala.


Haijawai Tokea

“nalikumbuka bao ambalo nililifunga  mwaka 1998 nikiwa na Timu ya Maji Maji ya Songea dhidi ya wekundu wa msimbazi Simba Toka Jijini Dar Es Salam, mara baada ya Kelvin Haule kuingiza crosi safi Toka winga ya kulia nami Sikufanya hajizi nikapiga shuti kali golini ambapo kilichotokea hata mimi sielewi niliupigaje ule mpira Golikipa Joseph Katuba akiwa amezubaa Pale Golini ule mpira Uligonga mara tatu mwamba wa juu na chini kwenye chaki mfurulizo na kutumbukia Kimiani,ni tukio la pekee ambayo mimi sikumbuki kama limewai tokea katika mechi zingine.


Mechi anayokumbuka

“Kipindi nipo yanga ilikuja timu toka afrika kusini [ Vall professional] ,ilikuwa mechi ngumu sana nakumbuka ilikuwa club bingwa Afrika raundi ya kwanza na mimi niliingia kipindi cha pili na katika mechi hiyo tulifanikiwa kupata ushindi wa bao 2-1,hali ambayo ilipelekea mchezo wa marudiano kuwa mgumu zaidi kwani ilitulazimu kusafiri hadi ugenini.

“Hatukukata tamaa  tukafanya mazoezi ya nguvu na tukajiweka fiti kwa ajiri ya mchezo wa marudiano,katka mchezo huo wa marudiano ambao ulichezwa nchini afrika kusini tulicheza kwa kujituma sana na hadi mwisho wa mchezo tuliambulia sare ya bao 1-1,ambapo bao la ugenini likatusogeza katika raundi ya pili ambayo tulipambana na timu kutoka visiwa vya usheli sheli.


Hakuwai humia


“Mungu mweza wa yote kwani kwa kipindi chote ambacho nilikuwa nikicheza kwa takribani miaka 15,sikuwai humia nilikuwa nacheza mpira bila matatizo yeyote zaidi tuu ya maumivu ya kawaida pindi mchezaji atokapo uwanjani kama ilivyokuwa kwa wachezaji wezangu.


Maoni yake kuhusu Timu ya taifa

“Timu ya taifa ya sasa imepiga hatua angalau wachezaji wanacheza mpira wa kuvutia ila kinachotakiwa kufanyika ni wachezaji kuwa wazalendo pamoja na Tff kuwa karibu Na timu kwa hali na mali.


Baada ya kustaafu

“kwa sasa mimi ni Askari Magereza kazi ambayo niliipata tangu nilipokuwa nikichezea Tanzania Prisons mara baada ya kuwapa masharti ya kutokuchezea timu yao hadi watakapo nipa kazi kweli walilidhia ombi langu na wakanifanyia mpango wa ajira ya kudumu.

“Sasa ivi nipo Singida ambapo Nimeoa na nina watoto wawili,pia nafanya kazi ya ufundi ambao niliusomea kabla ya kuanza kung’ara katka medani ya Soka.
Anasimulia David Mjanja ambaye kwa sasa yupo bize na kazi ya uaskari magereza ambapo kwa kipindi chote ambacho amecheza mpira alipata nafasi ya kuchezea timu ya taifa mara moja tu katika mechi ya kirafiki zidi ya Kenya wakati yupo Ushirika ya Moshi,pia amekili wazi kuwa alikuwa akisumbuliwa sana na Mohamed Mwameja wa Simba ambaye katika maisha yake ya soka alifanikiwa kumfunga bao moja pekee.

mwisho